51Թ

UNMISS yakarabati barabara jimboni Upper Nile, Sudan Kusini

Get monthly
e-newsletter

UNMISS yakarabati barabara jimboni Upper Nile, Sudan Kusini

UN News
5 May 2020
By: 
Mvua kubwa zilizosababisha mafuriko zimeharibu barabara na sasa wakazi wanatembea ndani ya maji ili kufikia maeneo yao huko Khor Adar.
UNMISS video
Mvua kubwa zilizosababisha mafuriko zimeharibu barabara na sasa wakazi wanatembea ndani ya maji ili kufikia maeneo yao huko Khor Adar.

Walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS wamekarabati barabara za kuunganisha maeneo ya Bunj na Melut yaliyoko mji wa Malakal jimboni Upper Nile, barabara ambazo ziliharibiwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa.

Walinda amani kutoka India wakiwa kwenye moja ya vitengo vya uhandisi mjini Malakal, walipowasili eneo la Khor Adar, walishuhudia jinsi mafuriko yalivyoharibu barabara yenye urefu wa kilometa 5 inayounganisha miji ya Bunj na Melut na Malakal katika jimbo hilo la Upper Nile.

Uharibifu huo ulisababisha wanawake wakiwa wamebeba mizigo mizito kichwani watembee ndani ya maji yenye kina kinachowafikia kiunoni huku wakiongozwa na watu waliojitolea.

Kutokana na uharibifu mkubwa, wahandisi walilazimika siyo tu kukarabati bali kujenga pia makalvati ili kuepusha uharibifu mwingine siku za usoni.

Mkuu wa kikosi cha uhandisi cha India kwenye, Luteni Kanali M.P.S. Ghai amesema kuwa,“katika jukumu hili, tulikuwa na maeneo manane magumu ya kushughulikia kuanzia mita 13 hadi mita 100. Kisha tukaweza kutumia uzoefu wetu kuweka makalvati na mabomba.”

Jima Agor Chai ambaye ni kiongozi wa jamii ya eneo hilo, ametoa shukrani zake kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwa msaada wao aliosema umefika kwa wakati akieleza kuwa,“barabara hii iliharibika katika maeneo saba kutokana na mafuriko nae neo hili ndio liliharibika zaidi. Ninawashukuru kwa kukarabati barabara. Ni mafanikio makubwa na wamekuja kuikoa jamii.”

Msimu wa mvua nchini Sudan Kusini ambao hudumu kwa takribani miezi 6 kila mwaka, huathiri zaidi maeneo ya ndani zaidi na kusababisha usafiri uwe mgumu.

Kwa mantiki hiyo, Sudan Kusini bado inategemea zaidi usafiri kwa njia ya anga, usafiri ambao hata hivyo ni gharama kubwa kwa jamii nyingi.

Pamoja na kukarabati barabara, walinda amani wa UNMISS wamejenga mifereji ya maji ili kufanikisha umwagiliaji mashambani na viwanja vya michezo kwa vijana.