Usitishwaji uhasama kote duniani utabadili mustakbali na kuleta neema kwa watoto milioni 250 wanaoishi katika maeneo yenye migogoro duniani limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na mkurugenzi mtendaji waHenrietta Fore akisema “Leo hii kuna watoto milioni 250 duniani kote wanaoishi katika maeneo ya vita. Kila mmoja wa Watoto hawa anataka pande kinzani kuitikia wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuweka silaha chini kama sehemu ya usitishwaji uhasama wa dunia nzima kupambana na mlipuko wa janga la virusi vya Corona auCOVID-19.Kila mmoja wa watoto hawa anataka hatimaye kuwa salama bila machafuko.”
Amesisitiza kwamba pande kinzani katika migogoro hazitoweza kupambana na COVID-19 wakati bado zinapigana zenyewe.
Ameongeza kuwa mwezi mmoja tangu wito wa Katibu Mkuu migogoro na machafuko bado yanaendelea nchini Afghanistan, Burkina faso, Libya, Mali, Syria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Ukraine na Yemen miongoni mwa nchi zingine.
Kusitisha uhasama kuna maanisha nini kwa watoto
Bi. Fore amesema “kwa watoto wanaoishi na jinamizi hili , usitishwaji uhasama utamaanisha tofauti kati ya uhai na kifo, utawalinda watoto dhidi ya kuuawa, kujeruhiwa au kulazimishwa kuzikimbia nyumba zao. Utasaidia kukomesha mashambulizi katika miundombinu muhimu kama vile vituo vya afya, maji na mifumo ya usafi, utafungua milango kwa wasiojiweza kupata fursa ya huduma kama za afya ambazo ni muhimu katika kukomesha mlipuko wa virusi vya Corona. Na pia utatoa fursa ya kujadiliana na pande kinzani katika mgogoro kuwaachilia salama watoto kutoka kwenye vikosi na makundi yenye silaha.”
Hata hivyo mkuu huyo wa UNICEF amesema kuna matumaini kwani pande husika katika machafuko kwenye nchi 11 tayari zimeahidi usitishaji uhasama wakati huu wa mlipuko wa COVIDI 19.
Kazi bado ipo kufikia lengo
Pamoja na matumaini hayo amesema bado kuna mengi ya kufanya kubadili Maisha ya watoto walioko maeneo ya vita“mosi ni kwa pande zote katika mzozo ni lazima kuandaa na kuheshimu muda wa mikataba ya usitishaji uhasama, pili mamlaka na makundi yanayodhibiti maeneo lazima yawezeshe fursa ya wahudumu wa kibinadamu ili kuwafikia watoto na familia zao kwa huduma muhimu, tatu majeshi na makundi yenye silaha hayapaswi kuwa kikwazo cha ufikishaji wa misaada au kuzuia watu wanaohitaji kupata huduma, na nne pande zote katika mzozo lazima ziachilie kila mtoto anayeshikiliwa mahabusu kwa kuhusiana na vita au usalama wa taifa.”
Bi. Fore amehitimisha kwa kusema kwamba wakati huu ambapo mamilioni ya watoto wako hatarini na mlipuko wa COVID-19 usitishwaji uhasama utakuwa kama mfano wa ushirikiano na mshikamano katika kupambana na janga hilo linalotishia binadamu wote na hususani wale wasiojiweza kabisa miongoni mwetu.
Usitishwaji huo utakuwa msingi wa amani ya kudumu ambayo ni kila kitu kwa watoto na mustakbali wao.