Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limetoa wito kwa mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ziimarishe uwepo wa jeshi na polisi kwenye maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo ili kunusuru maisha ya raia wanaoendelea kuteseka na kuuawa na vikundi vilivyojihami.
imetoa wito huo kwa kuzingatia ripoti za hivi karibuni kutoka majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini ya wakimbizi wa ndani wanashambuliwa, wanabakwa, kukatwa viungo na kuuawa hata pale wanapojaribu kurejea nyumbani baada ya hali kuwa shwari.
Msemaji wa UNHCR Babar Baloch akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo amesema vikundi vilivyojihami vinashambulia makazi ya wakimbizi wa ndani kwenye eneo la Djugu jimboni Ituri, Fizi na Mwenga jimboni Kivu Kusini na Masisi na Rutshuru katika jimbo la Kivu Kaskazini huku baadhi ya vitendo vya ukatili wa kingono vikidaiwa pia kufanywa na wanajeshi wa jeshi la serikali.
“Katika shambulio la tarehe 17 na 18 mwezi huu eneo la Djugu, watoto wawili, wanaume wawili na mwanamke mmoja waliuawa kikatili kwa kukatwa vichwa vyao kwa mapanga, zaidi ya nyumba 150 zilitiwa moto na watu waliokuwa na silaha kwenye vijiij viwili tofauti vinavyohifadhi wakimbizi. Na tarehe 23 mwezi huu takribani watu 5,000 walikimbia makazi yao katika siku moja kutoka jimbo la Kivu Kaskazini kufuatia mapigano kati ya vikundi viwili vilivyojihami mjini Mweso.vikundi hivyo vinapora shule ambako watu wanakimbilia kusaka hifadhi.”
Amekumbusha kuwa ghasia zinazoendelea zinakwamisha watu kupata huduma za afya na mashambulizi kwenye vituo vya afya yanafanya wanaopata dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi washindwe kupata huduma hiyo.
Hata hivyo amesema UNHCR na wadau wanaendelea kuhakikisha wanashirikiana na mamlaka husika kwenye majimbo hayo matatu ili kufanikisha kusafirisha manusura na wapate huduma za afya ndani ya saa 72.
Halikadhalika wanawapatia msaada wa malazi, vifaa na fedha wakimbizi hao wa ndani huku akikumbusha wahisaji kuchangia ombi la fedha la kusaidia DRC ambalo hadi sasa limechangiwa asilimia 21 ya dola milioni 168 zinazotakiwa na UNHCR kutekeleza operesheni zake.