Timu ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS imezuru eneo la Ras-Olo kwenye jimbo la Equatoria Magharibi ili kufuatilia ukiukwaji wa mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka jana. Wanawake katika jimbo hilo bado wanapitia ukatili mkubwa ikiwemo kutekwa na ubakaji.
Mapema alfakiri helkopta ya ikielekea kwenye eneo lenye rutuba nzuri ya kilimo la Ras-Olo jimboni Equatoria kwenda kushuhudia hali ya usalama na pia vitendo vya ukiuwaji wa mkataba wa amani.
Eneo hili kilimo ni uti wa mgongo sio tu kwa ajili ya chakula kwa wakazi wake bali pia kwa kujipatia kipato na kuzisaidia jamii za jirani.
Timu ya walindamani na wajumbe wa mkakati wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa mkataba wa amani (CTSMVM) wako hapa ili kutathimini hali na kutoa taarifa baada ya kufanya uchunguzi na kuzungumza na wakazi ambao wengi wamekuwa wakidai kufanyika ukatili na kuishi kwa kofu kutokana na makundi yenye silaha. Miongoni mwao ni Joice Levi ambaye anasema kuwa,“tunaishi hapa lakini tunakabiliwa na mtihani mkubwa wa kiusalama, wakati mwingine makundi yenye silaha yanakuja na kutewa vijana, yanachochea vita na kila wakati tuko kiguu na njia.”
Kwa mujibu wa UNMISS wanawake wa Ras-Olo ndio waathirika wakubwa wa machafuko. Na sio tu kwa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula lakini pia kukosa bidhaa nyingine za lazima na hakuna kituo cha afya hali ambayo inasababisha hatari kubwa hususan katika afya ya uzazi Joice mkazi wa eneo hili anathibitisha hilo"Huduma za dawa hazitoshi hasa ukizingatia kwamba zinaagizwa kutoka Juba na Maridi, na sasa kutokana na kutokuwepo usalama , na magari mengi kuchomwa moto njiani, hivyo hayawezi kutuletea madawa.”
Utekaji wa watu nao ni tatizo kubwa, Mary alitekwa yeye pamoja na wazazi wake na wakati wazazi wake waliachiliwa haraka yeye aliendelea kushikiliwa kwa siku kadhaa akishinikizwa kuwachotea maji na kuwapikia wapiganaji
“Walinichukua takribani saa saba usiku, na nilikuwa msituni pamoja nao kwa siku tatu. Walikuwa wanatutesa. Kila tulipokuwa tumeketi walitufunga kamba mikono yote na ikifika wakati wa kutembea walitufungua .”
Kwa sasa walindamani wa UNMISS wanaendelea kushika doria katika eneo hilo ili kukomesha machafuko na wanashirikiana kwa karibu na wahudumu wa misaada ya kibinadamu kuweza kuzisaidia jamii za eneo lote la Equatoria Magharibi.