Machafuko mapya katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa Nigeria yamewalazimisha watu 30,000 kufungasha virago na kukimbilia katika eneo la Maradi nchi jirani ya Niger ambako sasa wanapatiwa msaada na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.
Katika jimbo la Maradi nchini Niger lori la likiwasili na rundo la wakimbizi kutoka Nigeria ambao sasa wanapatiwa hifadhi katika eneo hili pamoja na misaada mingine muhimu kama chakula na malazi baada ya kufurushwa na mapigano yanayoendelea kwa miezi miwili sasa Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.
Licha ya janga la virusi vya Corona au COVID -19 lililosababisha mpaka baina ya nchi hizo mbili kufungwa kwa msaada wa UNHCR wameruhusiwa kuingia na wanasimulia madhila waliyopitia akiwemo Maigari Abara, aliyekuwa chifu wa Kijiji cha Gangara Nigeria,“walikuja takribani saa tisa adhuhuri na wakaanza kuua watu na mauaji yaliendelea hadi wakati wa swala ya jioni jua likizama. Watu walikuwa wanakimbia kila upande, na hadi sasa bado hatujui nini kilichotokea kwa baadhi ya wanavijiji.”
UNHCR inasema machafuko ya karibuni yamefanya idadi ya wakimbizi walioingia Niger kufikia 70,000, lakini pia ukosefu wa usalama mpakani umewafanya raia wa Niger 23,000 kuwa wakimbizi wa ndani.
Habsou ni mama wa watoto watano alikimbia pia kutoka Kijiji cha Gangara na akapotezana na mdogo wake mwenye watoto wanne aliyekuwa mjamzito na alipompata alikuwa tayari ameshakufa, na sasa analea watoto tisa wake na wa mdogo wake ,“uchungu wa kujifungua ulimshika na ulisababishwa na kukimbia, kiwewe na hofu na mauamivu yalikuwa makali sana, hakuweza kuishi. Nilipompata mtoto alikuwa bado anatembea tumboni lakini mdogo wangu alikwisha kufa.”
Sasa UNHCR inashirikiana na serikali ya Niger ili kuwahamisha wakimbizi 15,000 kuwapeleka katika vijiji vilivyopo kilometa 20 kutoka mpakani ambako huduma za maji, chakula, malazi na za afya zinaweza kutolewa kwa urahisi. Syldie Bizimana ni afisa UNHCR wa ulinzi wa wakimbizi , "katika vijiji vya mpakani hatukuweza kuhakikisha ulinzi kwa watu hawa, ufuatiliaji wa watoto, wanawake na maeneo yote ya ulinzi ilikuwa vigumu sana. Huko vijijini itakuwa fursa nzuri na rahisi kwa washirika wote wa misaada ambao tayari tunafanya nao kazi katika maeneo hayo.”