Mashirika ya Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO na lile la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo yametia saini makubaliano mapya ili kuimarisha huduma za afya ya umma kwa mamilioni ya watu waliolazimika kukimbia makwao.
Makubaliano haya mapya ya mashirika hayo yanapanua wigo wa yale yaliyotiwa saini mwaka 1997 na lengo muhimu mwaka huu litakuwa ni kusaidia juhudi zinazoendelea za kuwalinda watu milioni 70 waliolazimika kutawanywa, dhidi ya janga la virusi vya corona au COVID-19.
Mashirika hayo yanasema takribani watu milioni 26 kati ya hao ni wakimbizi na asilimia 80 kati ya wakimbizi hao wanahifadhiwa katika nchi za kipato cha chini na cha wastani ambazo mifumo yake ya afya ni duni. Na watu wengine milioni 40 ni wakimbizi wa ndani ambao wanahitaji msaada pia.
Kwa zaidi ya miaka 20nawamekuwa wakifanyakazi pamoja kuhakikisha wanalinda afya ya watu walio hatarini zaidi duniani.
Wameshirikiana kutoa huduma za afya kwa wakimbizi, huku wakichagiza ujumuishwaji wa wakimbizi na watu wasio na utaifa katika mipango ya afya ya kitaifa katika nchi zinazowahifadhi.
Leo hii mashirika hayo mawili yanafanyakazi bega kwa bega kupambana na mlipuko wa COVID-19 na kuhakikisha watu hao waliolazimika kukimbia makwao wanapata huduma za afya wanazohitaji, kuwalinda dhidi ya COVID-19 na changamoto zingine za kiafya.
Akizungumzia umuhimu wa ushirika huo mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema“Ushirikiano wa muda mrefu baina ya UNHCR na WHO ni muhimu sana kupambana na janga la corona na dharura zingine kila siku, unaimarisha na kuokoa maisha ya mamilioni ya watu waliolazimika kukimbia makwao. Ushirika wetu imara utanufaisha wakimbizi, waomba hifadhi, wakimbizi wa ndani na wale wasio na utaifa na unatumia vyema rasilimali za mashirika hayo mawili kwa ajili ya suluhu za afya ya umma kote duniani katika operesheni zetu.”
Naye mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema“Msingi wa mshikamano na lengo la kuwasaidia walio hatarini ndio nguzo ya kazi za mashirika haya mawili. Tuko bega kwa bega kulinda afya za watu wote waliolazimika kukimbia makwao na kuhakikisha kwamba wanapata huduma za afya wakati wanapozihitaji, na janga hili linaloendelea ni dhihirisho la umuhimu wa kufanyakazi Pamoja ili kupata mafanikio zaidi.”.
Mashirika hayo pia yanaungana na mfuko wa mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya COVID-19 uliozinduliwa mwezi Machi ili kuhakikisha janga la corona linatokomezwa lakini pia wanawalinda walio hatarini zaidi dhidi ya janga hilo.